Umuhimu wa Tunu na Maadili Katika Uongozi!

Subscribe the RSS Feed

Subscribe to Syndicate
6 August 2013 - 10:11pm -- charles

Mahusiano yote, mawasiliano na shuhuli katika maisha, iwe ni kwa watu binafsi, makampuni, au yote mawili, ni lazima yasimamiwe na kanuni na viwango. Kanuni hizi na viwango hujengewa kwenye msingi wa tunu ambazo husimamia maamuzi ya wale wanaohusika.

Mameneja na watendaji wana jukumu la msingi la kuweka na kusimamia viwango katika mashirika, na yafuatayo ni baadhi ya maeneo muhimu ambamo wajibu huu ni muhimu:

  1. Tunu za Shirika – Zaidi ya kuweka dira, mipango, na malengo ya shirika, uongozi una wajibu wa kuandaa tunu na miiko ya maadili itakayowaongoza wafanyakazi pamoja na viongozi. Mfumo wa tunu husaidia kulitambulisha shirika, kuwapa wafanyakazi hadidu za rejea kuhusu namna ambavyo wanapaswa kuenenda na kuwasiliana baina yao, kati yao na wateja na umma kwa ujumla.
  1. Wajibu wa Kisheria – Mashirika yote yanawajibika kutii sharia za nchi. Sharia hizi huathiri namna ambavyo biashara hufanyika kwa nia ya kulinda maslahi ya jamii, wadau, wateja na wabia. Utii wa sharia huathiri nana ambavyo tunapanga na kufanya maamuzi. Ni muhimu kwa uongozi kuzifahamu sheria zinazoathiri shuhuli zake na kutekeleza sera zinazosimamia shuhuli zake zinazozingatia sharia katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na utoaji wa taarifa na tahadhari ili kuwalinda wafanyakazi na mazingira.
  1. Wajibu kwa Wafanyakazi – Amali kubwa zaidi ya shirika lolote lile ni watu wanaolifanyia kazi shirika hilo; na kwa msingi huo wafanyakazi wasinyonywe wala kutendewa vibaya. Matokeo mazuri kwenye shirika hufikiwa endapo wafanyakazi watatoa ushirikiano na kufanya jitihada, na uongozi wa shirika ni lazima ujitahidi kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanatendewa  kwa haki na wanafaidi matunda ya ukuaji wa shirika pamoja na yale yatokanayo ili wajisikie kwamba na wao ni wadau katika mchakato wa kazi.
  1. Wajibu kwa Wateja – Biashara zinawajibu wa kuwa wakweli katika namna wanavyohusiana na walaji, ikiwa ni pamoja na kuwa wakweli katika muonekano na ufanyaji kazi wa bidhaa na uthabiti wa ubora wa huduma. Haya yakifanyika basi walaji wataiamini bidhaa husika na shirika litastawi kwa sababu wateja watarudi tena kwa manunuzi mengine.
  1. Wajibu kwa Jamii – Pamoja na ukweli kwamba jamii itakuwa inaheshimu na kupenda huduma zitolewazo na shirika, kuna hitaji muhimu kwa kampuni kuwajibika kwa jamii yote, zaidi ya zile huduma ambazo shirika hutoa kwa wateja wake. Huduma hiyo kwa jamii huweza kutolewa kwa mfumo wa kusaidia shuhuli mbalimbali za kijamii. Kugawana raslimali na jamii ambayo imechangia katika upatikanaji wa raslimali hizo husaidia katika kuboresha muonekano wa mzuri wa biashara husika, kukukuza sifa njema ya wafanyakazi na ari kuhusu kampuni husika.

Madhara mabaya ya kutokuwa na tunu na kutumia vibaya tunu zilizopo huonekana wazi katika mdororo wa uchumi wa dunia wa mwaka 2009/2009. Mdororo ule ulisababisha watu kupoteza kazi, watu kukosa imani na makampuni, mambo ambayo huleta madhara kwenye uchumi. Kinyume chake, kunapokuwepo na tunu bora biashara hushamiri na faida zake kusambaa katika Nyanja zote za biashara husika. Ninashauri kupitiwa kwa tunu na maadili ya kazi yaliyompo kwenye mashirika yenu. Ni kwa namna gani mnaweza kuyathamini na kuyaboresha?